Pages

Thursday, November 25, 2010

HUDUMA ZA TANESCO ZINAKATISHA TAMAA

Kwa muda mrefu nilikuwa nikisikia malalamiko ya Wananchi wenzangu dhidi ya huduma duni zinazotolewa na Tanesco nikawa siamini, maana tumezoea kuwa Watanzania ni watu wa kulalamika, sasa leo kwa macho yangu nimeshuhudia kile ambacho watu wengi walikuwa wakikilalamikia.
Jamani Tanesco panahitaji mabadiliko makubwa ili shirika hili liwe na tija na lifanye mambo yake kibiashara na kuwa shirika linaloiingizia Serikali faida badala ya kuwa mzigo.
Pale Tanesco kila kitu kimeoza, kuanzia customer care(jinsi mteja unavyokaribishwa) mpaka kwenye upatikanaji wa huduma yenyewe ya umeme.
Piga picha umeenda kulipia kuunganisha umeme, namaanisha wewe ni mteja mpya umelipelekea shirika pesa, sasa kinachotokea, kupata tu hilo faili lako ili uandikiwe ni kiasi gani cha pesa unatakiwa kwenda kulipa, ni mchakato kama wa masaa mawili hivi( kumbuka haupo peke yako).
Mtoa huduma wa kitengo hicho cha mafaili na kufanya makadirio ni mmoja tu ambaye anafanya kazi kwa kujisikia, pia mafaili yote ya wateja wapya bado yapo kwenye mfumo wa mgumu(manual) siyo computerised, kitu ambacho kinaifanya kazi ya kutafuta faili la mteja mmoja kuchukua muda mrefu, tofauti kama yangekuwa computerised ingekuwa kazi rahisi.(Tanesco wanahitaji kuwekeza kwenye eneo hili, uwezo wanao)
Ukifanikiwa kupata faili na kufanyiwa hayo makadirio inabidi tena ukae kwenye foleni nyingine ya kulipia, hapo unakutana na dada mwenye kisirani ambaye haoni hata umuhimu wa kumwambia mteja ni kiasi gani anatakiwa kulipia.
Zamu yako ya kulipia ikifika utaona anakutolea macho, wala hafanyi mawasiliano na wewe ambaye  ni mteja kukueleza ni kiasi gani unatakiwa kulipia. Akikuona unashangaa shangaaa ndio utamjua yeye ni nani.
Kwa siku ya leo tu, kwa muda niliokaa hapo kwenye jengo  la Tanesco kanda ya Ilala, nimepata hisia za kuwa kila mfanyakazi wa pale anajaribu kujenga mazingira ya kuonekana ni mtu fulani ili kuweka mazingira ya kumtisha mteja hatimaye kuwe na rushwa ya kupata huduma ambayo kimsingi ni haki ya mteja yeyote anayeingia pale kupata huduma bila ya manyanyaso wala bugudha.

Kilio changu ndio hiki jamani.

No comments:

Post a Comment